"

Primary Source Texts

Primary Source 1

Excerpt from an interview with “Maliki”

The following excerpt from my July 2009 interview with “Maliki” is from the prefatory conversation before we started talking about Popobawa. We met at a bar where he worked and I came back the next day to interview him during his break. I have edited the transcript slightly for clarity and to remove some unnecessary details.

1 MALIKI; Sawa?
2 KATRINA; Eh, sasa inarekodi.
3 MALIKI; Mimi naitwa Maliki Adili Suleiman.
4 KATRINA; A! Ni Maliki, si Malik?
5 MALIKI; A-a. Malik ni kifupi tu.
6 KATRINA; E, sawa.
7 MALIKI; Eeh, lakini ni Maliki. Mimi natokea visiwani Zanzibar.
8 KATRINA; Kisiwa kipi?
9 MALIKI; Unguja.
10 KATRINA; Sehemu gani?
11 MALIKI; Kaskazini Unguja. Inaitwa Mwanda. Nimezaliwa mwaka elfu moja mia tisa sabini na tisa.
12 KATRINA; O! Ni mdogo wangu! @
13 MALIKI; @Ndiyo. @@@
14 KATRINA; @@@
15 MALIKI; Eh, nina miaka thelathini thelathini. Ya, exactly thelathini thelathini.
16 KATRINA; Umeoa?
17 MALIKI; Mimi nilioa, lakini sasa niko mwenyewe. Tumetengana na mwanamke. Na nina mtoto, na nimesoma kule primary hadi sekondari, lakini bahati mbaya nilitoka katika familia maskini, hawakuweza kuniendeleza kimasomo. Nikatoka hapo nikaomba tena kusoma, wazazi wangu wakaniambia, “kwa kweli uwezo sisi hatuna kama unavyotuona ni maskini.” Basi nikajitahidi mwenyewe, nikaanza kufanya kazi hapa na pale. Nikapata pesa kidogo, nikaingia chuo, ingawa vile vile kumaliza ilikuwa ni taabu, kwa sababu sikuwa na pesa ya kutosha. Lakini—
18 KATRINA; Ilikuwa chuo cha aina gani?
19 MALIKI; Ni tourism. Chuo cha utalii.
20 KATRINA; Mmhh…
21 MALIKI; Baadaye nikaacha tena chuo. Nikakaa tena mitaani. And then nikarudi tena chuo. Nikamaliza masomo. Nikaanza kazi kwenye hoteli moja inaitwa Breezes Beach Club. Ni five star.
22 KATRINA; Mmhh.
23 MALIKI; Iko Unguja. Nilifanya kazi hapo kwa muda wa miaka mitatu. Kutoka hapo nikaenda kwenye hoteli nyingine. Inaitwa Pwani Ocean Station. Nikafanya kwa mwaka mmoja. Kipindi hiko tayari nishakuwa na mwanamke. Wakati naacha kazi Pwani Ocean nikaja huku mainland, I mean Dar es Salaam. Nikafanya kazi kwenye hoteli mmoja inaitwa Kilimanjaro Kruger Hotel.
24 KATRINA; Mm.
25 MALIKI; Nikafanya mwaka mmoja pale, mkataba ukaisha. Nikaacha tena pale, nikaja kufanya kazi Kumbwaya Beach Hotel. Wakati nafanya kazi kwenye Kumbwaya Hotel, ikatokea nafasi nyingine ya kazi, hapa, so nikaangalia maslahi yako wapi? I mean yah pesa nzuri. Nikaja TYC nikafanya interview, kwa sababu kule nilikuwa sina mkataba.
26 KATRINA; Mm.
27 MALIKI; Kwa hivyo nilikuwa nafanya kama’ … casual. Casual kwa Kiswahili inaitwa? Kibarua. Kwa hiyo nikaja hapa. Nikapata kazi. Nikapata mkataba. Sasa niko hapa nafanya kazi. Na naishi mwenyewe hapa Msasani. Nimepanga chumba kimoja. Yah hayo ndiyo maisha yangu yalivyo sasa.
28 KATRINA; Mm. Na bado una familia Unguja?
29 MALIKI; Watoto wangu wako Zanzibar. Yah wazazi wangu wote wawili wako kule Zanzibar. Unguja I mean, I mean. Wako kule. Naam tuna- nawasaidia. Kiasi ambacho nakipata mimi tunagawana. Ni bado maskini. Lakini nazidi kutafuta ili niokoe maisha ya wazee wangu pamoja na mimi. Ninachokipata kwa mwezi nawatumia. Na mimi nipo hapa natafuta. Lakini vile vile nishaomba nafasi ya masomo hapa. Kwa sababu kila mwaka anatoka mtu mmoja anaenda kusoma. Nasomea ufani ambayo nafanyia kazi. Kama mimi ni barman, naweza nikasoma nikapata— Shida yangu ni nichukue diploma.
30 KATRINA; Mm.
31 MALIKI; Ya utalii. Lakini kuna vizingiti huku na huku. Sasa nitajitahidi nitafute mwenyewe, niingie chuoni ili niongeze elimu ili maisha yangu kidogo yapande. Huo ndio— Hayo ndiyo maelezo ya maisha yangu yalivyo. Ndiyo.
32 KATRINA; Asante. Wewe ni: Mwislamu?
33 MALIKI; Mimi ni Mwislamu, ndiyo.
34 KATRINA; Na bado hapa barani unafuata dini? Yaani—
35 MALIKI; Wapi?
36 KATRINA; Hapa. Baada ya kuondoka Unguja bado uliendelea kufuata dini hapa?
37 MALIKI; Um, kwa kweli mimi tangia niko kule Zanzibar, naweza kusema kipindi nikiwa mdogo, wakati naishi na wazee wangu nilikuwa nafuata dini vizuri. Na naijua. Nimesoma. Nimesoma Korani. Lakini nikaacha kufuata dini kwa sababu ya kazi zangu.
38 KATRINA; Mm.
39 MALIKI; Sisi Waislamu kuna baadhi ya vitu hatutakiwi hata kushika. Kama pombe.
40 KATRINA; Eeh.
41 MALIKI; Nguruwe. Lakini mazingira ya kazi yamesababisha mimi nishindwe kufuata dini. Na kwa kweli mpaka leo sifuati dini.
42 KATRINA; Mm.
43 MALIKI; Mmm. Nasikitika sana lakini, kwa sababu ya maisha, sio kingine. Mm. Ni hivyo.
44 KATRINA; Asante.
45 MALIKI; @ @ @Asante @na @wewe.
46 KATRINA; Unamaswali yo yote juu ya maisha yangu au?
47 MALIKI; Ya.
48 KATRINA; Kabla ya kuanza na hadithi?
49 MALIKI; Ya, nitapenda mimi nijue kidogo.
50 KATRINA; Haya.
51 MALIKI; Maisha yako yako vipi?
52 KATRINA; Haya. Mimi nilizaliwa Marekani, jimbo la New York.
53 MALIKI; Ndiyo.
54 KATRINA; Katika mji mkubwa wa New York.
55 MALIKI; Sawa.
56 KATRINA; Lakini nilipokuwa na miaka mitano hivi tulihamia jimbo la Massachusetts, ambapo babangu alizaliwa. Kwa sababu mamake alifariki, na tulienda kumtunza babake ambaye alikuwa mzee sana.
57 MALIKI; Ndiyo.
58 KATRINA; Na nilikuwa mtoto pekee wa wazazi wangu.
59 MALIKI; Ndiyo.
60 KATRINA; Kwa hiyo tuliondoka mji mkubwa tukaenda kijijini. Kijiji hicho kilikuwa na watu elfu nne tu, nafikiri. Na baada ya miaka michache wazazi wangu walitengana. Kwa hivyo mimi na mama yangu tulihama. Tukaenda jimbo lingine, lakini baada ya mwaka mmoja au miwili hivi tulirudi jimbo la Massachusetts ili nikae karibu na babangu.
61 MALIKI; Ndiyo.
62 KATRINA; Na baada ya kumaliza shule ya sekondari nilihamia pekee yangu jimbo la Iowa, kwenda chuo kikuu
63 MALIKI; Ndiyo.
64 KATRINA; Na wakati wa chuo kikuu niliamua kwenda Afrika, kusoma kwa nusu ya mwaka. Nikaenda Zimbabwe. Nilianza kujifunza lugha ya Kishona.
65 MALIKI; Ndiyo.
66 KATRINA; Na niliamua kuendelea na fasihi za Kiafrika ama lugha za Kiafrika, hasa Kishona. Lakini nilipofika chuo kikuu kingine ili kupata digrii za pili na tatu, profesa wa Kishona alikuwa amestaafu mwaka huo. Kwa hivyo walimu wengine walisema “A, itabidi usome Kiswahili badala ya Kishona.”
67 MALIKI; @
68 KATRINA; Nikaanza Kiswahili, lakini sikuvutiwa sana nacho kwa sababu nilikuwa sijafika Tanzania au Kenya.
69 MALIKI; A, ndiyo.
70 KATRINA; Lakini baada ya miaka miwili ya kusoma Kiswahili nilipata nafasi ya kuja Tanzania. Nilikaa Unguja kwa wiki nane, pamoja na familia ya Waislamu. Na nilisoma Kiswahili pale Taasisi.
71 MALIKI; Ndiyo.
72 KATRINA; Halafu baada ya hapo nimerudi mara nyingi. Sasa kila mwaka au miaka miwili narudi.
73 MALIKI; Ndiyo.
74 KATRINA; Naenda kuwatembelea familia
75 MALIKI; Mmm.
76 KATRINA; ya Unguja. Au nakuja Dar es Salaam. Kwa hiyo nina marafiki hapa.
77 MALIKI; Ndiyo.
78 KATRINA; Nimefanya utafiti mwingine kuhusu muziki kama Bongo Flava na kadhalika.
79 MALIKI; Mm.
80 KATRINA; Lakini sasa nimeamua kufuatilia hadithi za popobawa.
81 MALIKI; @ @ @ Sawa. Umeolewa?
82 KATRINA; Niliolewa lakini nimeachana na mume wangu.
83 MALIKI; Na una mtoto?
84 KATRINA; Eh tuna mtoto mmoja. Ana miaka saba.
85 MALIKI; Kwa hiyo sasa uko mwenyewe.
86 KATRINA; Eh.
87 MALIKI; Sawa. Nashukuru.

License

Icon for the Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License

Dini Afrika ya Mashariki Copyright © 2017 by Katrina Daly Thompson is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License, except where otherwise noted.

Share This Book