Main Body
Kutumia Vitenzi Vilivyonyambuliwa Kusimulia
Kusimulia Kuhusu Maonyesho ya Muziki
Shughuli ya Mwanafunzi: Hii ni bendi ya Sauti Sol. Unaweza kusoma zaidi kuhusu bendi hii hapa: https://sw.wikipedia.org/wiki/Sauti_Sol. Umehudhuria maonyesho yake jijini Nairobi. Simulia mbele ya darasa uliyoyaona kwa kutumia vitenzi vilivyonyambuliwa katika kauli mbalimbali za mnyambuliko wa vitenzi. Zingatia maelezo na mifano ya vitenzi vilivyonyambuliwa iliyotolewa hapa chini.
Mnyambuliko wa Vitenzi
Kunyambua ni kurefusha kitu. Vitenzi vya Kiswahili huweza kunyambuliwa kwa viambishi tamati ili kuleta maana mbalimbali. Viambishi ni nini? Viambishi ni vipashio vinavyowekwa kwenye mzizi wa neno ili kupanua maana au kuunda neno jipya.
Vitenzi vya Kiswahili hunyambuliwa katika kauli mbalimbali kama vile kutendea, kutendwa, kutendewa, kutendana, n.k.
- KUTENDA – ndiyo hali ya kawaida ya kitenzi, kabla ya kunyambuliwa. Mifano: cheza, ona, cheka, enda, sikia, tembea, kaa, imba, n.k.
- KUTENDEA – viambishi -i-, -e-, -le-, -li- huongezwa kwenye mzizi. Ikiwa mzizi una irabu a, i, au u basi hunyambuliwa kwa -i-. Iwapo mzizi una irabu e na o, hunyambuliwa kwa -e-. Iwapo mzizi unaishia kwa irabu, basi l huongezewa na huchukua e au i kutegemea irabu ya mwisho kwenye mzizi. Maana zinazoletwa ni: (a) kitendo kinafanywa kwa naiba ya mtu mwingine – Maria ananioshea nguo. (b) kitendo kinamfaidi au kumhasiri mtu – Amenipikia chakula. (c) kifaa au ala inayotumika kufanyia kitendo – Mimi nilisafiria basi (nilisafiri kwa basi). (d) kuonyesha mahali kitendo kilitendekea – Walisomea darasani. (e) kuonyesha kitendo kinaelekezwa kwa mtu mwingine – Mtoto alimwendea mamake – Mtoto alielekea alipokuwa mamake.
Kitenzi Mzizi Kiambishi Kitenzi Kilichonyambuliwa
a. imba imb- -i- imbia
b. ona on- -e- onea
c. enda end- -e- endea
d. tembea tembe- -le- tembelea
e. kaa ka- -li- kalia
- KUTENDWA – hutumiwa kuonyesha kuna mtu au kitu kinachoathiriwa na kitenzi moja kwa moja. Kimbishi kitumiwacho ni -w-. Mifano: a) Ngoma ilichezwa mpaka che. b) Viti vilipangwa katika mstari. c) Wimbo uliimbwa kwa dakika tano. d) Watu waliopigana walishikwa na polisi.
- KUTENDEWA – huonyesha kitu au mtu anapokea kitendo kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Huonyesha pia kitendo kimetendwa kwa niaba au manufaa ya mtu mwingine. Huonyesha sababu za kutendwa kwa kitendo vilevile. Viambishi vitumikavyo ni -ew-/-iw-/-liw-/-lew- kutegemea mzizi kama nilivyoeleza katika kauli ya KUTENDEA . Mifano: a) Wanabendi wa Sauti Sol walipokelewa kwa furaha. (kutokana na POKEA – poke-lew-a) b) Tulichezewa nyimbo kumi na bendi ile. c) Msichana yule aliimbiwa wimbo na mpenzi wake. d) Viti vilivyokaliwa vilikuwa vichache.
- KUTENDEKA – huonyesha kuwezekana au kufanyika kwa kitendo bila kutaja mtendaji wa kitendo. viambishi vyake ni -ik-/-ek-/-lik-/-lek-/-k-. mifano: a) Mlango ulifungika kabla sijaingia ukumbini. (fung-ik-a) b) Dirisha lilifunguka nilipolisukuma.(fungu-k-a) c) Ukumbi ulijaa watu kupita kiasi na haungekalika. (ka-lik-a) d) Ngoma ile inachezeka kwa urahisi. (chez-ek-a) e) Ukumbi ungechomeka kama wazimamoto hawangefika mapema. (chom-ek-a)
- KUTENDANA – watu/vikundi viwili huhusika ambapo mtu au kikundi kimoja kinatendea kingine/mwingine kitendo, na hicho kingine/mwingine anamtendea yule wa kwanza. Kiambishi kitumikacho ni -an-. mifano: a) Wageni walisalimiana walipowasili. b) Tuliimbiana wimbo wa Sauti Sol. c) Wanabendi wale wamejuana kwa muda mrefu.