Main Body

Onyesho la tatu: Muhtasari

Katika sehemu hii, wanawake wanaamua kuacha tofauti zao na chuki. Wanaamua kuja pamoja ili kuinua Nguzo Mama. Wanapojaribu mara ya kwanza, Nguzo Mama inaonyesha dalili za kuinuka.  Lakini mara tu kabla ya kuinuka, baadhi yao wanaanza kupoteza umakini katika kazi na kufuatilia mambo yasiyo ya muhimu. Bi. Moja anaacha kuvuta Nguzo Mama na kwenda kununua kanga. Baada ya muda mfupi, Bi. Pili anasikia sauti ya mtoto wake akilia kutoka nyumbani. Anaacha kazi ya kuinua Nguzo Mama na kukimbia kwenda nyumbani kumuona mwanae. Mara Bi. Sita anamuona hawara wake MAGANGA kwa mbali. Anaacha kuinua Nguzo Mama na kumfuata. Lakini MAGANGA ni mumewe Bi. Tano. Kwa hivyo Bi. Tano anaacha kazi pia na kuwafuata Bi. Sita na MAGANGA. Bi. Tano anamuita Bi. Sita kuwa yeye ni malaya kwa sababu anachukua mume wake. Kunakuwa na vurugu kati ya wawili hawa hadi wanaanza kutukanana na kupigana. Hawarudi tena kuinua Nguzo Mama. Baada ya muda mfupi mume wa Bi. Tatu anapita na Volvo kumchukua Bi. Tatu waende kwenye sherehe. Bi. Tatu anasema lazima amfuate mumewe kwa sababu ndiye anayemtegemea kwa matumizi yote, yeye hana kazi. Anaogopa kuachwa.

Sasa wanabaki wanawake watatu peke yao: Bi. Nne, Bi. Saba na Bi. Nane. Lakini Bi. Nne anakumbuka kwamba anahitaji kuhudhuria kikao cha viongozi. Kwa hivyo anaacha kazi pia na kuondoka. Punde Bi. Saba anawaona shemeji zake Kiando na Makange wamebeba kitanda na vitu vingine vya nyumba. Anaacha kuinua Nguzo Mama na kuwafuata. Kiando na Makange wanachukua vitu hivi kwa sababu ni vya kaka yao aliyeaga dunia. Walianaza kwa kuchukua shamba na watoto. Sasa wamechukua kila kitu nyumbani. Vilevile wanataka kupewa pesa alizoacha kaka yao. Bi. Saba anakabiliana nao lakini anashindwa, anaanza kulia. Anaacha kufanya kazi na kwenda nyumbani. Bi. Nane anabaki mwenyewe kuinua Nguzo Mama Anajaribu lakini anashindwa. Anaona kwamba anapoteza nguvu zake bure. Anaacha. Nguzo Mama inabaki imelala pale pale.

License

Materials for Swahili Learners Copyright © by kdthomp3. All Rights Reserved.