Main Body

Muhtasari: Onyesho la Nne

La mgambo anatangaza kuwa wahenga wameamua kuichukua Nguzo Mama iwapo Wanapatata wameshindwa kuisimamisha. Wametoa kiasi cha siku tatu.  Kama Nguzo Mama haitasimama, wataipeleka kijiji kingine ambapo itasimamishwa.  Au, wataiweka kuwa kumbukumbu. Wanawake wanaposikia hivi, wanachangamka tena. Lakini wanaume wao wanashikilia msimamo wao wa awali. Wanaongeza kuwa Nguzo Mama ikisimama wanawake wataanza kudharau wanaume. Wanawake wanaanza tena kuiinua Nguzo Mama. Kila mmoja anajaribu mbinu zake. Lakini katika jukwaa ilipolala Nguzo Mama, yupo Chizi. Wanawake wanapokuja mmoja mmoja kuisifu Nguzo Mama, Chizi anakashifu tabia zao. Tabia zao ndizo zinawafanya washindwe kuinua Nguzo Mama.

Kulingana na Chizi, wanawake wengine ni wazembe. Hawafanyi kazi ili kupata rasilimali ya kuboresha maisha yao. Wanapendekeza mbinu ambazo hawana uwezo wa kuzitekelezaWengine wananyanyaswa na waume zao. Kwa mfano, Bi. Pili anashindwa kujiendeleza kwa sababu ya mumewe. Kila anapofanya kazi na kupata pesa, mumewe anazichukua. Wanawake walio na uwezo, kama vile Bi. Tatu, ni bahili, wana dharau na mioyo michafu. Kwa sababu hii, maendeleo ya jamii yanakuwa vigumu kufanywa. Viongozi kama vile Bi. Nne wanaazimia kutekeleza miradi ambayo ni hafifu. Anasema zaidi bila kutenda. Chizi anaona kwamba angalau kila mwanamke ana mapungufu ambayo yanamzuia kufanikisha maendeleo.

Hata hivyo, wanawake tena wanakusanyika ili kujaribu kusimamisha Nguzo Mama kwa pamoja. Wanajitahidi lakini Nguzo Mama haisimami. Wanashindwa kuelewana ni maarifa gani watumie kufanya kazi hii. Wanaendelea kuinua lakini wanashindwa.

License

Materials for Swahili Learners Copyright © by kdthomp3. All Rights Reserved.