Mapambazuko ya Machweo

Mzee Makucha na Mzee Makutwa ni marafiki, ambao wamestaafu na umri wao umesonga. Hata hivyo, urafiki wao uliokolea awali sasa umepungua, umebaki tu ule wa kujuliana hali. Mzee Makutwa anaonekana akizurura mtaani na gari lake baada ya kustaafu, wala hakuna ajuaye shughuli zake, hata Mzee Makucha. Anaonekana tu kila mara akiwabeba vijana garini, wala haijulikani anawapeleka wapi. Mkewe Makucha, Bi Macheo anamsaili mumewe kuhusiana na hili lakini hapati taarifa yoyote. Makutwa anajinaki kuwa hawezi kuishi maisha ya kutaabika hata kama amestaafu. Bi. Macheo anamshauri mumewe akomeshe urafiki na Mzee Makutwa, lakini mumewe anamweleza kuwa urafiki uliobaki kati yao ni wa salamu tu.

Mzee Makucha anauza vitafunio kwenye makutano ya barabara baada ya kustaafu kutoka kazi yake alipopigwa kalamu. Anafanya kazi na shirika la reli lakini linasambaratika baada yake kuachishwa kazi, hivyo juhudi zake kwenda mahakamani ni bure. Akiwa kazini kwake(kuuza vitafunio), anashangazwa na kazi anayofanya Makutwa, ambaye anatangamana na vijana kila uchao wala hana hata muda wa kuwasabahi wazee wenzake.

Mzee Makutwa anafika katika kazi ya Mzee Makucha na kutapakaza vumbi kwenye vitafunio vyake kwa gari lake akilipiga breki. Anamkejeli Makucha, akimwambia kuwa anafaa kujipumzisha nyumbani na kazi hiyo kuachia vijana. Lakini Makucha anamsisitizia kuwa yuko sawa nayo, kuliko yeye anayezurura mitaani na vijana. Anamdhihaki kuhusu bintiye aliyetoroshwa na Mhindi, huku akimkumbusha afurahie maisha licha ya matatizo. Mashaka ya Makucha kuhusu kazi afanyayo Makutwa yanazidi.

Vijana wawili, Dai na Sai wananunua kashata kwa Makucha na kuelezana kuhusu taabu za maisha baada ya kufuzu na kukosa kazi. Wanaamua kujaribu bahati yao na gari la probox linalozunguka likikusanya vijana. Makucha anajua bila shaka ni gari la Makutwa. Gari linapofika wanalipungia mkono na kuingia. Linaendeshwa na kijana sasa hivi, sio Makutwa.

Makucha anamwita mkewe kuchukua vitu vyake na kuchukua teksi kulifuata gari lile. Wanasafiri hadi wanapoingia kwenye mgodi wa kisiri uliofichwa katika mazingira makavu. Anaingia kwenye mgodi na kushuhudia jinsi vijana wanavyodhalilishwa humo kwa kazi ya kutafuta madini. Anarudi tena na kuwadanganya walinzi kuwa anamtaka Mzee Makutwa, ambaye huku anaitwa Mzee Mamboleo. Anawaaga akidai atamfuatilia nyumbani.

Anarudi mjini Kazakamba na kuripoti polisi, ambao wanaandamana naye hadi kwenye lile pango. Wanamkuta Mzee Makutwa akikagua mgodi. Anatokomea pangoni na kupotelea humo, hadi polisi wanapomrushia vitoza machozi. Anatoka akikohoa na kufungwa. Anamlaumu Mzee Makucha kwa kumwendea kinyume, lakini naye anamwambia haki ndio muhimu. Hatimaye anatupwa korokoroni kwa kosa la jinai.

Mzee Makucha anapokea zawadi ya hundi ya pesa kutoka kwa tajiri mmoja anayeendeleza miradi ya maendeleo kwa vijana. Anayaona haya kama mapambazuko mapya, licha ya maisha yake kuwa katika machweo.

License

Materials for Swahili Learners Copyright © by kdthomp3. All Rights Reserved.