Sura ya kumi na tatu [13]

88 Muhtasari na mchezo: Sura ya kumi na tatu

Muhtasari


Wakati Charles na Rosa walipokwenda nyumbani kuwaona wazazi wao ulikuwa wakati mbaya sana katika sehemu ya kaskazini Tanzania. Maafa yalitokea kila mahali. Ugonjwa mpya ulizuka. Wakerewe waliuita ‘Ugonjwa wa miguu’, lakini kwa kweli ilikuwa ni aina ya malaria. Watu wengi walikufa kwa sababu ya ugonjwa huu. Hata mjomba wa Charles, Ndalo, alikufa.

Rosa na Charles walipokuwa wakikaribia mji wa Ndalo, Charles alimpa Rosa barua “juu ya mpango wote kuhusu uchumba wetu na siku ya kufunga ndoa,” alisema. Alimwomba asiisome mpaka usiku. Wote wawili wakaenda mazikoni. Ndalo alizikwa. Mji wote ulikuwa na huzuni. Wakati huo huo mtu fulani alisikika akiimba wimbo. Alikuwa Zakaria. Alianza kupiga kelele za kilevi, akapanda juu ya kaburi, akaanza kusema, “Uhuru wananchi! Mimi nikiwa mwenyekiti wa walevi hapa…”, lakini hakumaliza. Alipigwa kwa mkuki kifuani, akafa. Regina alipomwona Zakaria ameuawa, naye alikufa palepale.

Wakati huu Rosa hakuwapo. Alikwenda nyumbani kusoma barua ya Charles. Alipoifungua, hakuamini alichosoma. “Ha! Rosa, kweli wewe ulikuwa bikira. Unafikiri baada ya kufahamu kwamba ulichezewa sana huko Morogoro, mimi ninaweza kukuoa! Ha! Dada yangu, sahau! Haiwezekani hata kwa mizinga! Hata kama ukiwa wa bure!” Rosa machozi yalimtelemka mpaka kifuani. Kuishi aliona hawezi. Alichukua chupa na kuisagasaga juu ya jiwe. Akaweka ule ungaunga wa vipande vya chupa ndani ya glasi. Aliweka maji, akayanywa. Alianza kuona nyota, nyota machoni. Alifikiri juu ya malezi mabaya ya baba yake na jinsi alivyochungwa kiasi cha kushindwa kuutumia uhuru alipoupata.

Honorata alipoingia, Rosa alikuwa hapumui tena. Honorata alianguka chini na kuzimia. Watu waliposikia juu ya vifo hivi, walikuja nyumbani kwa Zakaria. Hata wale ambao hawakuwa na ujamaa na Zakaria walisikitika. Regina alilazwa kati ya Rosa na Zakaria. Ye yote aliyeangalia uso wa Rosa alisema, “Sijaona msichana aliyesumbuka maishani kama huyu!” Maiti hawa walioshwa na kuzikwa.

Charles alipewa barua ya Rosa iliyookotwa na waosha maiti. Iliandikwa na Rosa, ikisema, “Ninajiua kwa ajili yako. Kuoa bikira ni bahati tu, wala si kitu cha kutafuta.” Charles alisumbuliwa na dhamiri yake. Aliona ukweli ndani ya maneno yale, lakini hata hivyo alihitaji bikira. Baada ya siku chache alikwenda mjini Kisubi kusomea ubruda. Flora pamoja na mchumba wake John walikata shauri kwamba watawatunza wadogo wa Flora.

Mchezo wa Kuigiza

Chukulia kwamba wewe na mwanafunzi mwenzako ni wanaharakati wa kutetea haki za mapenzi. Mnashiriki katika majadiliano kwenye radio ya taifa kuhusu mswada wa mapenzi na mna maoni tofauti kuhusu mapenzi. Andika insha ya ukurusa moja ya kutoa hoja zako huku ukimshawishi mwenzako akuunge mkono.

 

License

Icon for the Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License

Mazoezi ya Rosa Mistika Copyright © by Magdalena Hauner is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License, except where otherwise noted.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.