Sura ya tisa [9]

61 Muhtasari: Sura ya tisa

Muhtasari


Siku moja Rosa alikaribishwa na mwalimu mkuu wa chuo cha Morogoro. Alichukua muda mrefu kujitayarisha. Alipoingia chumba cha Mwalimu Thomas, aliulizwa, “Unatumia nini, Martin au VAT 69?” Rosa na Mwalimu Thomas walianza kunywa mvinyo. Baada ya kunywa kidogo, mwalimu alisema kwamba walimu wengine wanataka kumfukuza Rosa shule, lakini yeye atamhakikishia kwamba hatafukuzwa. Baadaye waliendelea kunywa. Walikunywa, wakaanza kucheza dansi, mpaka mwalimu akamwomba Rosa avue nguo wakalale, kwani saa zilikuwa zimekwenda. Kila mmoja moyo ulikuwa ukimdunda. Walibusiana tena na tena.

Mwalimu alipotaka kumshika Rosa, Rosa alimshika mkono, akasema, “Si kawaida yangu.” Yaani, alisema hataki kulala naye siku ya kwanza. Mwishowe, Thomas akaamka akitaka kulala kitanda kingine. Ghafla Rosa alimshika, akamkumbatia. Thomas sasa alikuwa hafahamu yuko wapi. Alisema maneno mengi. Aliapa kwamba Rosa hatafukuzwa shule. Rosa aliona kwamba ameshinda. Lakini, siku za mwizi ni arobaini. Walisikia mlango ukigongwa, ukapasuliwa. Mke wa mwalimu aliingia na shoka lake mkononi. Alimshika Rosa, akamwangusha chini, akamwuma sikio na kulitoa kabisa! Rosa alikimbia huyooo! Alipopona, Rosa alivaa kitambaa kichwani siku zote.

Rosa sasa alijulikana kama mke wa mwalimu mkuu. Ilikuwa vigumu kumfukuza shule. Wanafunzi walianza kumchukia kiasi cha kumtemea mate. Rosa alianza kuona kwamba baba yake ndiye aliyefanya makosa katika malezi ya binti zake. Akakata shauri kutomsikiliza baba yake.

Siku moja Mkuu wa Wilaya, kaka yake Thereza, alikuja kumchukua Rosa “beach”. Motokaa yake ilipofika, Zakaria alimfokea sana Mkuu wa Wilaya. Alimwambia Rosa, “Usitoe pua yako nje!” Lakini Rosa pia alikasirika, akasema maneno makali: “Kila wakati unatuchunga. Unafikiri utatuoa wewe?!” Zakaria, akajibu, “Rosa, tangu leo wewe si mtoto wangu.” Rosa akijibu, “Tangu leo wewe si baba yangu.” Aliingia ndani ya motokaa na kwenda zake “beach”. Alirudi nyumbani baada ya siku mbili.

Zakaria na rafiki yake Ndalo waliongea kwa muda mrefu juu ya vijana na tabia zao “mbaya”. Walifikiri ingalikuwa bora kama wasingaliwapeleka watoto wao shuleni. Walisikitika kwamba ulimwengu uligeuka.

Rosa naye aliporudi nyumbani alionywa na Regina afunge mizigo aondoke upesi kabla ya Zakaria kurudi nyumbani. Rosa hakukataa. Alifunga mizigo na kwenda kukaa kwa mama yake wa ubatizo.

Maswali

 

License

Icon for the Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License

Mazoezi ya Rosa Mistika Copyright © by Magdalena Hauner is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License, except where otherwise noted.

Share This Book

Feedback/Errata

Comments are closed.